Onyesho hilo limevunja rekodi ya uchangamfu baada ya wakazi hao kuanza kumshangilia kuanzia msanii wa kwanza hadi wa mwisho huku onyesho likiisha saa sita usiku na kuwaacha mashabiki wakiwa bado na hamu ya kusikia zaidi.
Kwa Dodoma ziara ya muziki ya Kili ilijumuisha wanamuziki zaidi ya tisa na burudani ilidumu kwa saa sita huku msanii wa kwanza kupanda jukwaani akiwa ni Khadija Kopa aliyetumbuiza kwa takriban dakika 45.
Ukiweka pembeni ukongwe wake, kwa mara ya kwanza malkia huyo wa taarab Tanzania alipanda jukwaani na wasindikizaji wa kike ambao walisababisha onyesho lake kuwa changamfu kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Ukiachana na Khadija Kopa wasanii waliofuata wote walifanya kazi nzuri ya kuhakikisha kwamba mashabiki wao wanakata kiu yao ya burudani na awamu ya kwanza ilimalizwa na Mwasiti, Rich Mavoko, Shilole na Christian Bella.
Awamu ya pili ya burudani ilifunguliwa na MwanaFA ambaye alitumbuiza kwa takriban dakika 50 akafuatwa na Izzo B, Ben Pol na kisha onyesho likafungwa kwa mara nyingine tena na kundi matata la Hip Hop liitwalo Weusi kutoka Arusha.
“Kwa kweli watu wa Dodoma wamechangamka sana…hata wamenifanya nifikiri niko kwetu Mbeya…nimependa sana uchangamfu huu umenipa nguvu ya kufanya vizuri zaidi jukwaani,” alisema Izzo B, mmoja wa wasanii wa tamasha hilo.
Baadhi ya wakazi wa Dodoma waliishukuru Kilimanjaro Premium Lager kwa kuwaletea burudani kubwa kwa bei nafuu ya Sh. 3,000 kwani pia walipata bia ya bure kwa wale wenye umri zaidi ya miaka 18.
“Hii haiwezi kutokea kabisa…kuwaona wasanii wote hawa wenye majina kwa Sh.3,000 na bia juu…sio jambo la kawaida hawa wadhamini ni wa kuuungwa mkono kabisa kwani wanasaidia sana katika kukuza muziki wetu na pia wanawajali wasanii,” alisema Paso Elias, mkazi wa Dodoma.
Ziara hii inaratibiwa na kampuni za East Africa TV na Radio, Executive Solutions, Integrated Communications, Aggrey and Clifford na Aim Group.
Ziara ya muziki ya Kili inatarajiwa kuendelea Jumamosi ijayo huku wasanii zaidi ya 10 wanatarajiwa kuelekea mkoani Kigoma.
0 comments:
Post a Comment