Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
Kelele ambazo zimepazwa na watu wa kada mbalimbali
nchini dhidi ya mchakato wa Katiba mpya zimeifanya Kamati Kuu ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kukutana kwa dharura, huku kukiwa na taarifa ndani
ya chama hicho kuwa kuna hoja zinazokinzana juu ya kuendelea au
kusitishwa kwa muda kwa Bunge Maalum la Katiba.
Kikao hicho kinachokutana mjini hapa leo, inadaiwa kitajadili miito ya
wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakitoa kauli za kumtaka Rais Jakaya
Kikwete aliahirishe Bunge Maalum la Katiba linaloendelea na vikao vyake
hadi hapo maridhiano yatakapopatikana baina ya CCM na wajumbe wanaounda
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Bunge hilo lililorejea katika ngwe ya pili Agosti 5, mwaka huu baada ya
kuahirishwa Aprili 25, mwaka huu kupisha mkutano wa bajeti sasa
linahudhuriwa na wajumbe wengi kutoka CCM, wachache kutoka kundi la 201
na wachache zaidi kutoka vyama vidogo vya siasa.
Wajumbe wengi wa vyama vinavyounda Ukawa vya Chadema, CUF na
NCCR-Mageuzi walitoka nje ya Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu
wakilalamikia mambo mbalimbali ikiwamo Bunge hilo kuweka kando Rasimu ya
Katiba iliyoandaliwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya
uenyekiti Jaji Mstaafu Joseph Warioba na kujadili rasimu mbadala ya
CCM.
Wadau hao wanapendekeza kwamba Bunge hilo liahirishwe hadi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kumalizika.
Chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya chama hicho, kimeeleza kuwa
kikao hicho cha leo kilitanguliwa jana jioni na kikao kingine cha
Sekretarieti ambacho hupanga ajenda zitakazojadiliwa.
“Baadhi ya viongozi wa juu, tayari wameshawasili akiwamo Makamu
Mwenyekiti, Philip Mangula ambaye alishinda jana kutwa nzima hapa
ofisini akijaribu kuandaa mazingira, Pia nimemuona Nape Nnauye, lakini
Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM yeye ataingia kesho (leo)
asubuhi kwa ndege…Na jioni hii (jana) tunampokea Katibu Mkuu
(Abdurahaman Kinana),” kilisema chanzo hicho.
NIPASHE lilimshuhudia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akiwasili mjini hapa
majira ya saa 8:36 mchana akitokea jijini Dar es Salaam na kukutana
faragha na baadhi ya mawaziri katika ukumbi wa Mkapa.
Wajumbe wa kamati kuu waliotakiwa kuwa wamefika Dodoma kwa ajili ya
kikao hicho ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na
Bunge), William Lukuvi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na
Uratibu) Stephen Wassira; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Profesa Anna Tibaijuka; Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Slaa;
Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi na Naibu Waziri wa
Maendeleo ya Wanawake, Jinsia na Watoto, Pindi Chana.
Wengine ni Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Dk. Hussein Mwinyi; Dk. Salim Ahmed Salim, Profesa Makame
Mbarawa, Dk. Maua Daftari, Hadija Aboud na Waziri wa Nchi, Ofisi Makamu
wa Rais (Muungano), Samia Hassan Suluhu.
Taarifa za kuaminika zinaeleza kuwa miito ya wadau inayotolewa hivi sasa
kila kona ya nchi, ikimtaka Rais Kikwete aliahirishe bunge hilo,
imekuwa ikimpasua kichwa na kwamba kilichozungumzwa na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Jaji Frederick Werema mwishoni mwa wiki iliyopita alisema
ni maono ya serikali kukubaliana na wadau, lakini kwa sharti la kuwaanda
kisaikolojia Watanzania.
“Zipo ajenda nyingine ambazo nadhani zitajadiliwa, lakini kubwa ni hoja
zinazotolewa na baadhi ya waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, shinikizo la vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) kutaka maridhiano na Rais Kikwete baada ya kususia Bunge Maalum
la Katiba, kupokea taarifa ya Kamati ya Maadili ambayo ilipewa kazi ya
kufanya marejeo na kuangalia utekelezaji wa adhabu kwa makada wake
waliofungiwa kwa muda wa mwaka mmoja,” chanzo hicho kilisema.
Baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa kutokana na joto la kisiasa kupanda
hususani shinikizo la kutaka kutafutwa kwa maridhiano na kuahirishwa kwa
Bunge hilo vinaweza kuwafanya CCM walegeze msimamo wa kuendelea na
vikao vya Bunge Maalum.
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye,
alipozungumza na NIPASHE jana jioni, alisema kwamba ajenda ya kikao
hicho ni kupokea taarifa ya maendeleo ya mchakato wa Bunge Maalum la
Katiba.
Nape alisema kikao hicho ni mfululizo wa vikao vya Kamati Kuu na siyo cha dharura ila ni kamati maalum.
Nape aliongeza kuwa katika kikao hicho watapeana taarifa kuhusu mambo yanayoendelea katika Bunge Maalum la Katiba.
Nape alikanusha taarifa kwamba kikao hicho pia kitajadili suala la
wanachama wake sita waliopewa dhabu ya mwaka mmoja kutojihusisha na
shughuli za chama hicho na kuwa chini ya uangalizi kutokana na tuhuma
kuwa walianza kufanya kampeni kabla ya muda rasmi kinyume cha kanuni na
taratibu za CCM.
Wanachama hao waliochukuliwa hatua hiyo Februari mwaka huu ni mawaziri
wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya
Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Uratibu na Mahusiano), Stephen Wassira; Naibu waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa
Sengerema, William Ngeleja.
“Wanaosema kuja ajenda kuhusu adhabu ni uzushi, ni maneno ya mitaani,”
alisema Nape na kuongeza kuwa watu wasijenge hali ya wasiwasi na kwamba
chama hicho kitatoa taarifa rasmi baada ya kikao hicho.